Vita vya Ghaza bado havijamalizika, lakini sauti za kutaka Benjamin Netanyahu atimuliwe madarakani zinazidi kupasua anga ya kisiasa na kiutawala ya Israel. Hata kabla ya vita vya Ghaza pia, hali haikuwa nzuri kwa Netanyahu.
Wakazi wa utawala wa Kizayuni walimiminika mabarabarani kumpinga Netanyahu tangu siku za awali kabisa za kuunda serikali yake na maandamano hayo yanaendelea hadi hivi sasa. Netanyahu amelemewa na kesi nne kubwa za ufisadi, huku njama zake za kufanya mapinduzi ndani ya mfumo wa mahakama wa utawala wa Kizayuni zikimwaga pertroli ndani ya moto uliokuwa unarindima wa kutaka aburuzwe mahakamani kujibu mashitaka mazito yanayomkabili yeye na watu wa familia yake.
Baada ya kuanza vita vya Ghaza tarehe 7 Agosti 2023, jinamizi limezidi kumwandama Netanyahu kwani si tu ameshindwa kuwakomboa mateka wa Kizayuni walioko mikononi mwa wanamuqawama wa Ghaza, lakini pia ameshindwa kuiangamiza Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS kama alivyoahidi. Hayo yamezidisha maandamano ya kutaka Netanyahu atimuliwe madarakani. Ehud Olmet, waziri mkuu wa zamani wa utawala wa Kizayuni anasisitiza kuwa, lazima Netanyahu ango'ke. Anasema, Netanyahu ni muongo, ni tapeli na ni mdanganyifu mkubwa na kwamba mbinu anazotumia kujinufaisha kisiasa ni ukidhabi uliofurutu ada. Olmet anasema, Netanyahu anapaswa kutambua kuwa, hawezi kufikia malengo yake aliyoyatangaza kwenye vita vya Ghaza.
Mashinikizo ya kutaka Netanyahu afurushwe madarakani yameongezeka zaidi katika wiki za hivi karibuni. Baadhi ya marafiki wa Netanyahu ndani ya baraza lake la vita la mawaziri nao pia wanataka waziri mkuu huyo wa utawala wa Kizayuni atimuliwe madarakani. Mizozo ya mara kwa mara ndani ya baraza hilo la mawaziri inaripotiwa kila leo na moja ya sababu za mizozo hiyo ni kutaka Netanyahu afukuzwe.
Gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronoth limeripoti kuwa, baada ya kipigo kikali ulichopata utawala wa Kizayuni kutoka kwa wanamuqawama wa Palestina tarehe 7 Oktoba, waziri mkuu wa Israel amepoteza uungaji mkono hata kutoka kwa wafuasi na waitifaki wake wakuu.
342/